Sunday, 8 March 2020

Mbinu za Kuwa Penzini Bila Presha.

Mbinu za Kuwa Penzini Bila Presha.
Mbinu za Kuwa Penzini Bila Presha.
MAISHA ya uhusiano kwa sasa yana changamoto nyingi. Watu wanaishi kwenye makelele ya kila aina. Huyu anagombana na mwenzi wake kwa sababu ya usaliti, mwingine anagombana na mwenza wake kutokana na ukorofi tu binafsi.

Hii inatokana na jinsi kizazi cha sasa kinavyojirahisisha kufanya mambo kwa mazoea. Kuchukulia vitu kawaidakawaida tu. Mathalan, mtu ni mume wa mtu, lakini nje ana michepuko kama yote.

Anaona ni jambo la kawaida tu yeye kuchepuka. Mtu ni mke wa mtu, lakini naye anakuwa na michepuko nje. Mbaya zaidi si kwamba anafanya kwa siri, mazingira ambayo anayafanya yapo wazi kabisa. Mtu anajiona mjanja, ananufaika na penzi la ziada ilhali analo lililo halali. Ndiyo maana ninasema, kizazi hiki cha sasa kimeharibika.

Imefika mahali kila mtu anamlaumu mwenzake. Mke anamlaumu mume, kwamba haridhiki, lakini mume naye anamtupia lawama mke kwamba naye ni walewale. Ile imani na heshima kwamba huyu ni mke au mume wa mtu inazidi kuporomoka siku hadi siku.

Inafika mahali unashindwa kutofautisha huyu ni mke wa mtu au bado hajaolewa. Mavazi anayovaa mke wa mtu ni kama vile anatafuta mabwana kwa nguvu.

Mke wa mtu anatembea nusu utupu, unategemea nini? Jibu ni rahisi tu, anajiuza! Haridhiki na yule aliyenaye. Anawinda masoko mengine ambayo anaamini atanufaika nayo. Hapo ndipo tulipofikia.

Mazingira tuliyopo si salama tena, ni hatari hata kwa afya. Ndiyo maana leo nataka tujifunze kwamba, maisha yalivyo tunapaswa kujua namna bora ya kuishi ili kuhakikisha tunakuwa salama sisi na vizazi vijavyo.

Wewe ambaye umeamua kwa dhati kuingia kwenye maisha ya uhusiano, unapaswa kujitambua. Ujijue kwamba ni mume au mke wa mtu, hupaswi kucheza na moyo wa mwenzako. Usalama wa mwenzako unatembea nao wewe.

Heshima ya mwenza wako upo nayo wewe. Ukijirahisisha ni kwamba unajidhalilisha, lakini kubwa kabisa unahatarisha afya yako na ya mwenza wako. Kila mmoja akilitambua hilo, atamlinda mwenzake. Atajiheshimu ili kulinda heshima ya ndoa yenu. Hakutakuwa na sababu ya kufuatiliana sana.

Mnapofuatiliana sana, wakati mwingine mnajisababishia ‘stresi’ zisizokuwa na lazima. Hakuna ulazima wa mke kuwa anapekuwa mara kwa mara simu ya mumewe. Lakini pia mume naye asitumie nafasi hiyo kufanya mambo ya kijinga maana mwisho wa siku madhara yataonekana. Unaposaliti ipo siku utajulikana tu.

Ukijulikana itakuwa ni mwanzo wa ugomvi, itakuwa ni mwanzo wa kelele zisizokuwa na kichwa wala miguu. Mjengee mwenzako mazingira ya kumuamini, anayeaminiwa naye aheshimu. Kuchunguzana sana ni kusababisha kero zisizokuwa na ulazima.

Kila mmoja wenu atambue kwamba ana dhamana ya uhai wa mwenzake. Asijirahisishe na kama mwenzako akishindwa kujiheshimu na kufanya mambo ambayo yanakudhalilisha au kukuhatarishia afya, basi ni bora mtu huyo kuachana naye kuliko kuendelea kuvumilia matatizo yanayoweza kukatisha uhai. Ifike mahali mheshimiane, mpendane kwa dhati na muishi kama marafiki.

Mshirikishane kuhusu suala hilo na muishi katika upendo wa dhati. Somo hilo likiwaingia kwa dhati, hakuna hata mmoja kati yenu anayeweza kuleta mzaha kwenye uhusiano wenu.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.